MakalaMilele FmSwahili

Babake Careen: Careen aliiba pesa kumpa Louis Otieno kabla ya kifo chake.

Aliyekuwa mtangazaji kwenye runinga Louis Otieno ameshtumiwa kwa kumchochea aliyekuwa mpenzi wake marehemu Careen Chepchumba kukopa vitita vya pesa ili kugharimia maisha aliyokuwa akiishi Louis. Babake Chepchumba, Hosea Kili amesema bintiye alisababisha deni ya milioni 3 pesa kwa jumla alizotumia kwa kodi ya nyumba ya Louis, matibabu nchini na ng’ambo.
Aidha Kili aliambia mahakama kwamba bintiye alimnunulia Louis gari aina ya Range Rover baada ya kuliuza lake aina ya VW. Mahakama pia ilielezewa kuwa kabla ya kifo chake Chepchumba alielezea hofu yake kutokana na vitisho vya Louis na hakutaka utangamano naye kutokana na hofu ya vitisho vyake.
Babake marehemu ambaye ni mkurugenzi wa County Pension Fund aliambia mahakama kuwa shida ilichipuka punde tu Louis alipohamia makazi yake Chepchumba mwaka wa 2011. Alisema kuwa Chepchumba mara ya kwanza alikana kuwa na uhusiano na Louis japo baadaye alikubali kuwa wapenzi, baada ya kuwekewa mtego na familia na kufumaniwa. Babake alipokuwa akimjibiza bintiye Louis anasemekana kutoka nje ya nyumba yake kushuhudia kilichokuwa kikiendelea.
Kili amesema kutoka hiyo siku Chepchumba alianza kumwibia pesa tabia ambayo hakuwahi kuhusika wala kuonesha maishani. Chepchumba baadaye anasemekana kuchukua laki sita kutoka babake na alipoulizwa alisema alikuwa amechukua kali nne kugharimia matibabu ya Louis.
Mahakama vile vile iliambiwa kuwa mapema Chepchumba aliacha kuishi kwa babake na kuenda kuishi kivyake na kuidanganya familia yake kuwa nyumba hiyo ilikuwa Amboseli ilhali ilikuwa karibu na walikokuwa wakiishi na baada ya wiki kadhaa Kili alipokea ripoti kutoka kwa watu kadhaa kuwa bintiye alikuwa amechukua deni kutoka kwao akitoa sababu za kila aina.
Chepchumba aliyepatikana akiwa amefariki Februari 14 2012, alikuwa amejichimbia kaburi la aibu kutokana na mikopo aliyokuwa amechukua. Hata hivyo, alifichua kuwa alikuwa amemnunulia Louis Range Rover KBQ 122S baada ya kuliuza gari lake na kulipa pesa taslimu.
Baada ya hayo yote kujulikana alikubali kulipa kiasi fulani ya mikopo kwa kukubali mshahara wake kukatwa na babake angegharimia kulipa mengine. Kwa machozi aliomba msamaha na kulilia familia yake kumkubali arejee nyumbani na aliahidi kuandikisha ripoti kwenye kituo cha polisi kesho yake.
Ndugu yake alimpeleka hadi kwake usiku bila kujua ndio ilikuwa ni mara yao ya mwisho kumwona baada ya familia yake kujaribu kumfikia kwa simu bila mafanikio. Alipatikana akiwa ameaga alikokuwa anaishi. Babake anasema alipomwona bintiye akilala kitandani alishuku jambo lisilokuwa la kawaida lilikuwa limempata na kuita polisi kuchunguza kifo chake na matokeo ya kilichosababisha kifo kilionesha alikuwa amenyongwa. Louis anatarajiwa kutoa ushahidi kuhusiana na kisa hicho kwenye kikao kingine cha mahakama.

Show More

Related Articles

Close