HabariMilele FmSwahili

Gavana Sonko aachiliwa kwa dhamana ya Ksh 15m pesa taslimu

Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 15 pesa taslimu au bondi ya shilingi milioni 30 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho katika kesi inayomkabili ya ubadhirifu wa shilingi milioni 357.

Mahakama ya ufisadi chini ya hakimu mkuu Douglas Ogoti imetoa masharti ambayo gavana huyo na washtakiwa wenza wafaa kufuata ikiwa ni pamoja na kutofika ofisini mwake bila kuandamana na afisa anayechunguza kesi yake.

Gavana wa Nairobi, Mike Sonko angali katika seli za mahakama ya Milimani hapa Nairobi akisubiri kukamilishwa mchakato wa kulipia dhamana ya shilingi milioni kumi na tano pesa taslimu, ili kuachiliwa huru. Aidha usalama umeimarishwa nje ya majengo ya mahakama hiyo gavana Sonko akisubiriwa kuondoka.

Katika uamuzi wa kumuachilia kwa dhamana hakimu wa mahakama ya ufisadi Douglas Ogoti aliridhia ombi la Sonko kupitia wakili Cecil Miller, kuitaka mahakama imruhusu kurejea hospitalini kuendelea na matibabu wakati wanaposhughulikia uamuzi wa kumwachilia kwa dhamana.

Gavana Sonko anayekabiliwa na mashtaka ya wizi wa zaidi ya shilingi milioni 357 , pamoja na washukiwa wenzake wameagizwa kuwasilisha stakabadhi zao mahakamani huku idara ya uhamiaji ikitakiwa kuhakikisha kuwa hawataondoka nchini wakati kesi hiyo inapoendelea.

Pia wamezuiwa dhidi ya kuwasiliana kwa njia yoyote na mashahidi, wala kuizungumzia kesi hiyo katika mitandao ya kijamii.

washukiwa wengine  wananne miongoni mwa kumi na sita walioshtakiwa pamoja na Sonko wameachiliwa kwa bondi ya shilingi milioni tatu, mdhamini wa kiasi sawa na hicho au shilingi milioni tatu pesa taslimu

Show More

Related Articles

Close