MakalaMilele FmSwahili

Kila afungapo bao Ramsey, mtu maarufu hufariki!

Laana ya imani yenye ushirikina kwamba kila afungapo Ramsey bao mtu maarufu hufariki imeendelea baada ya kifo cha mke wa aliyekuwa rais wa Marekani Ronald Reagan, Bi Nancy Reagan kutokea baada ya bao lake Aaron Ramsey wa timu ya ligi kuu Uingereza Arsenal.
Kwa miaka minane iliyopita watu kadhaa mashuhuri wameugua au kupata majeraha siku moja tu kila afungapo bao nyota huyu wa taifa la Wales. Hisia hizi za imani ya kishirikina zimeongezeka baada ya Ramsey kuifungia Arsenal bao la kwanza la mechi katika kipindi cha kwanza dhidi ya Totenham Jumamosi iliyopita.
Kabla ya mechi ya Jumamosi laana hii ilikuwa imeibua maswali ya utani ya ni nani atakayekuwa mwathiriwa endapo atafunga bao Ramsey. Ni wazi sasa kwamba kilichokuwa kikidhaniwa kuwa sadfa tu kimekuwa ukweli mchungu wa kuduwaza kutokana na msururu wa matukio haya!
Ramsey japo anachukulia swala hilo kuwa imani ya fikra zitokanazo na matukio ya kisadfa tu, amegusia kwa ucheshi akisema kwamba angaa baadhi ya waathiriwa wanaotokana na makali ya guu lake la kulia wamekuwa na ubaya fulani, hivyo huenda hiyo ilikuwa adhabu yao.
Imani hii ilimpata mwathiriwa wake wa kwanza mwaka wa 2008, alipoifunga Fernabahce kisha gwiji wa kitamaduni David Lloyd Meredith akafa. Mwaka wa 2009 Ramsey aliifunga Portsmouth kisha aliyekuwa seneta wa Marekani Ted Kennedy akafariki hata baada ya kuhepa visa, visanga na mikosi tele za kuhusiana na kifo, ila hakuweza kuukwepa mkwaju wa safari ya jongomeo kutoka Ramsey.
Hata hivyo watu walianza kupigia jicho angavu sana kwa makini laana hii ya mwanabunduki huyu alipoihasiri Manchester United na kusababisha kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Al-Qaeda Osama Bin Laden siku moja baadaye. Mwaka huo huo tu, mambo yalichacha sana Ramsey alipofunga dhidi ya Spurs kisha mwasisi wa kampuni ya Apple Steve Jobs alipofariki siku moja baadaye.
Baadaye mwezi huo alipoiaga dunia Jobs kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi alinaswa na waasi kisha kuuliwa baada ya bao la Aaron Ramsey dhidi ya Sunderland kabla ya mwimbaji gwiji wa muziki wa soul Whitney Houston kupatikana akiwa ameaga bafuni.
Mwaka 2013, Ramsey alirejea nyumbani Cardiff akatia langoni magoli mawili dhidi ya timu yake ya awali na siku hiyo hiyo tu gwiji wa filamu Fast and Furious Paul Walker alihusika katika ajali akiendesha gari lake la kifahari la Porsche na kufariki.
Miezi michache baadaye mwuigizaji Robin Williams alipatikana amefariki baada ya Ramsey kufunga dhidi ya Manchester City kwenye dimba la Community Shield.
Licha ya guu lake kuwapa kheri sana watu wenye umaarufu mwaka wa 2015, magoli yake ya 2016 yameonekana kurejesha laana hiyo.
Kufuatia goli lake dhidi ya Sunderland, David Bowie alifariki siku moja baadaye. Licha ya imani hii kutozingatiwa sana enzi ya sasa, utani mwingi kutokana na matukio hayo umewabumbuaza wengi.
Walakini, Gwiji wa Harry Potter alipofariki siku nne tu baada ya Ramsey kuisaidia Arsenal kuipiga Liverpool, ndipo maswali ya nani atakayeangukia mtego wake yalipochacha kila afungapo bao. Ndiposa alipofunga wikendi iliyopita ilikuwa wazi kwamba alikuwa amemtia Bi Nancy Reagan kwenye orodha ya waliozikwa kutokana na uzito na makali ya guu lake la kulia na kutia tamati mojawapo ya ndoa zilizotokana na mapenzi ya kihistoria katika urais wa Marekani.

Show More

Related Articles

Close