MakalaMilele FmSwahili

Mfahamu Shujaa Collins Injera

Collins Injera mchezaji wa timu ya taifa ya raga wachezaji saba na kumi na watano upande alizaliwa mwaka wa 1986. Anafahamika sana kwa kushiriki misururu ya wachezaji saba upande na anasifika sana katika ufungaji wa trai nyingi duniani akiwa anashikilia nafasi ya pili baada ya Santiago Gomez Cora wa Argentina aliyestaafu aliye na jumla ya trai 230 Injera akiwa na 225 muingereza Ben Gollings mstaafu pia akiwa wa tatu na 220.

Injera alianza kupiga raga akiwa shule ya upili ya Vihiga. Baada ya mahafali yake 2005 alijiunga na timu ya jeshi ya Ulinzi RFC iliyokuwa ikishiriki ligi ya Kenya Cup kabla ya timu hiyo kuvunjiliwa mbali naye akahamia timu ya Mwamba RFC ya Nairobi anayoichezea nafasi ya winga.

Sasa akiwa kiungo muhimu wa Kenya7s alijiunga na timu hiyo kwa mara ya kwanza 2006 msururu wa Dubai kisha kucheza 2009 kombe la dunia la raga ambapo Kenya ilifika nusu fainali. Alikuwa mfungaji bora 2008-2009 msururu wa IRB Sevens World Series na trai 42. Alifunga alama 210 na kumaliza wa pili nyuma ya Ben Gollings wa Uingereza.

Injera pia alichezea timu ya wachezaji 15 upande namba 11 mgongoni mwaka 2011 mechi za kufuzu kombe la dunia. Februari 2013, aling’olewa kwenye timu ya wachezaji saba upande na mkataba wake kufutiliwa mbali na kocha Mike Friday. Hii ilikuwa ni kutokana na tofauti za kimkataba kati ya timu yake ya Mwamba RFC na timu ya taifa ya wachezaji saba upande.

Injera aliteuliwa kuwania mchezaji bora wa IRB Sevens Player of the Year 2009 tuzo iliyonyakuliwa na Ollie Phillips wa Uingereza. Injera alishinda mwanaspoti wa mwaka Kenya 2009 kisha 2010 alituzwa tuzo ya rais ya Order of Golden Warriors (OGW) akiwa na ndugu yake mkubwa Humphrey Kayange kutokana na kutia fora 2008-2009 IRB Sevens World Series.

Nduguye Humphrey amekuwa nahodha kabla ya kumpokeza shujaa Andrew Amonde ambaye naibu wake ni bingwa Collins Injera. Ndugu yao mdogo Michael naye hupigia raga timu ya taifa ya raga. Injera amesomea shahada ya mawasiliano kutoka Kenya College for Communication Technology (KCCT) iliyo sasa chuo kikuu cha multimedia.

Injera 29 baba wa watoto wawili sasa ametia nakshi ubora wa ukali kwa kuteuliwa mchezaji bora katika msururu wa dunia wa IRB awamu iliyopigwa kwa mara ya kwanza Singapore. Hii ni baada ya kuiongoza Kenya kupiga mibabe Fiji wanaoongoza misururu yote kileleni kwa alama 30-7.

Ushindi wa Kenya umeipa alama 22 nyingi zaidi kuweza kuwahi kupata katika msururu wowote na kusonga hadi nafasi ya 7 kwa alama 85 kwenye mashindano inayoshirikisha timu 16.

Show More

Related Articles

Close