BurudaniMilele FmSwahili

Nyota Ndogo apata nyota kuu ya ndoa

Nyota wa burudani kutoka pwani Nyota Ndogo amekuwa mteja asiyepatikana kwa waliommezea mate na kuotea pingu za maisha naye. Hii ni baada ya malkia huyu wa kutumbuiza kwa uimbaji kumwachisha ukapera mpenzi wake kutoka Denmark Henning Nielsen kwa kufunga ndoa pamoja nyumbani kwao Voi wikendi.

Wawili hao walivishana pete kwenye harusi iliyohudhuriwa na jamaa zao, marafiki, wasanii na watu mashuhuri hususan katika ulingo wa burudani baada ya miaka miwili ya kuchumbiana.

Mwanaisha Abdalla maarufu kwa lakabu yake Nyota Ndogo anatamba sana kutokana na muziki wake ulio na miguso ya kitaarab kama; Watu na Viatu, Dunia, Mpenzi na mengineyo mengi.

Ana wana wawili msichana na mvulana kutoka ndoa yake ya awali na mtayarishi wa muziki yaani produsa kutoka Mombasa K-Shot na anapania kuwa na watoto zaidi kulingana na matamshi yake ya siku za kabla ya ndoa yake.

Ni wazi kuwa Nyota amefurahia sana hatua aliyopiga maishani kufunga ndoa walakini ndoa hii imepokea kejeli kutoka kwa ndugu yake mwanaSwahili Jazz Juma Tutu aliyeelezea kutofurahia ndoa ya Nyota na mpenzi wake aliyemtaja kuwa mzee kupita kiasi na amemwoa ili awe tu mkidhi wa mahitaji yake yaani ‘sponsor.’

Wiki iliyopita Juma alimwelekezea lawama na kumshtumu Nyota kwa kutuma maafisa wa upelelezi CID kumpiga. Juma ametia doa ndoa ya dadake akisema amemwoa ‘babu.’

Show More

Related Articles

Close