HabariMilele FmSwahili

Ripoti ya BBI yazidi kuibua hisia mseto

Ni bayana sasa kwamba huenda ripoti ya BBI imezindua ukurasa mpya wa kisiasa nchini.

Hii ni kutokana na kauli za wanasiasa wenye hisia mseto wanaohisi huenda ripoti hiyo ikachangia mgawanyiko na uhasama nchini badala ya utangamano uliolengwa.

Kinara wa ODM Raila Odinga anasisitiza kuandaliwa kura ya maoni ili kuafikia utekelezwaji wa ripoti ya BBI. Raila na wanasiasa wanaomuunga mkono wanapinga ripoti hiyo kuidhinishwa na bunge kwa hofu itatupiliwa mbali .Hatua hii sasa inatarajiwa kuendelea kuwagawanya wakenya licha ya Rais Uhuru Kenyatta kutaka hilo kukoma

Inadaiwa wana ODM walitaka nafasi ya waziri mkuu mwenye mamlaka na sio ile aliyependekezwa kwenye ripoti hiyo ,lakini sasa wanasema suluhu ni kura ya maoni.

Usemi wao ukiridhiwa na wabunge wa mrengo wa kieleweke wanaosema hawana imani na wenzao wa mrengo wa tangatanga wanaomuunga mkono naibu rais William Ruto kwani wanaweza kuiangusha ripoti hiyo iwapo itawasilishwa bungeni.

Lakini mbunge wa Taveta aliye mwandani wa Ruto Dr Naomi Shaban anasema taifa halihitaji kura ya maoni na mapendekezo ya BBI yanaweza kutekelezwa kupitia bunge.

Rais Kenyatta hajasema jinsi ripoti hiyo itatekelezwa badala yake anawataka wakenya kuisoma kabla ya kongamano la kitaifa mwezi Januari mwakani,sasa ishara zote zikiwa yeye ndiye atakua na uamuzi wa mwisho.

 

Show More

Related Articles

Close