MichezoMilele FmSwahili

Stephen Keshi aliyekuwa nahodha na kocha wa Nigeria afariki

Aliyekuwa mchezaji wa timu ya soka ya Nigeria na aliyepanda ngazi na kuwa kocha wa timu ya taifa Stephen Keshi amefariki. Aidha Keshi aliwahi kuwa mkufunzi wa timu za Togo na Mali. Usakataji kandanda wake ulikuwa pamoja na kupigia gozi klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji. Keshi anaripotiwa kupata mshtuko wa moyo na kufariki kwa mujibu wa mojawapo ya vyombo vya habari nchini Nigeria. Akiwa mchezaji, Keshi alikuwa kiungo muhimu sana kwa timu ya Super Eagles kikosi kilichoshinda kombe la ubingwa barani Afrika mwaka 1994 japo baadaye kukosa kwa tundu la sindano tu kuingia katika robo fainali ya kombe la dunia mwaka huo huo. Aliifundisha Super Eagles kwa misimu mitatu na kuwaongoza kutwaa ubingwa wa Afrika 2013 Afrika Kusini. Vile vile aliwaongoza vijana wake kuingia katika raundi ya 16 katika kombe la dunia 2014 Brazil. Hata hivyo, hakuongezewa muda wa kuhudumu katika kandarasi yake baada ya kipute hicho cha kombe la dunia, ambapo alirejea tu kuiongoza Super Eagles kwa zamu ya mechi moja moja tu, baada ya Nigeria kufeli kufuzu kwa ubingwa wa Afrika 2015. Alipigwa kalamu kutoka kuwa kocha wa zamu walakini alirejeshwa baada ya rais Goodluck Jonathan kuingilia kati utata uliopo, kabla ya kufutwa kabisa mwezi Julai.

Show More

Related Articles

Close