BurudaniMilele FmSwahili

Wikendi ya WAMBUI: BOB COLLYMORE, DADDY OWEN wawatia pingu za maisha Wambui

Wikendi iliyopita imekuwa ni wikendi iliyofana ya kutosha hususan kwa akina dada wawili wanaotambulika kwa majina ya Wambui. Alitangulia mwanamuziki wa nyimbo za injili Daddy Owen maarufu kwa jina la kisanii Papa Fololo siku ya Jumamosi kwa kukata kauli ya maisha ya kumtia pingu za maisha mpenzi wake wa muda mrefu Bi Farida Wambui.
Daddy Owen aliasi ukapera na kujitosa katika ligi kuu ya wanandoa siku moja tu kabla ya bwanyenye wa Safaricom Bob Collymore kumpa mkono wake wa pete ambaye pia amemchumbia kwa muda Bi Wambui Kamiru.
Wakati ndege wakifurahia wikendi hii kwa kunofoa minofu iliyosazwa na waalikwa kwenye harusi hizi mbili safari ya akina dada ambao haswa wamekuwa wakiwamezea mate Bob na Owen hatimaye imefikia ukingoni na hawana la ziada ila kukata tamaa tu!
Bob amekuwa mteja kutoka Jumapili ya jana kwa wale waliolenga japa angaa kijipande cha M-PESA toka kwake huku naye Daddy Owen akiwa tayari keshampata ‘Defender’ wake hivyo waliokuwa na mate ya kummezea hawana budi ila kujimezea tu!
Hata hivyo imekuwa ni wikendi ya kukata na mashoka si shoka kwa dada hao wawili ambao sadfa imewapata kuwa na majina sawa na kuoleka wikendi sawa na waume wawili wanaotambulika katika nyanja na fani zao kitajika.
Mmmh……shabash……la ziada kwetu kuwaelekezea kwao daima tu tunawaombea zaidi ya kuwatakia maisha mema ya kheri katika pingu zao za maisha.

Show More

Related Articles

Close